Fulgence Kayishema, Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari huenda atahukumiwa nchini Rwanda - Serge Brammertz | | Haba...
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ofisi ya mwendesha mashtaka ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari, IRMCT iliyoko Arusha Tanzania, Serge Brammertz ameeleza kuwa Fulgence Kayishema, mmoja wa watuhumiwa vinara waliokuwa wanasakwa zaidi kwa kuhusika na mauaji ya kimbari nchini Rwanda, aliyekamatwa juzi Mei ishirini na nne (24) huko Paarl nchini Afrika Kusini huenda akapelekwa nchini Rwanda kukabiliana na mkono wa sheria kutokana na tuhuma za kushiriki kuwaua watu zaidi ya elfu mbili (2000) wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka elfu moja mia tisa tisini na nne (1994). Anold Kayanda amezungumza na Mwendesha Mashitaka huyo na kutuandalia makala ifuatayo.
Ni Mwendesha Mashitaka Mkuu huyo, ofisi ya Mwendesha mashitaka ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari ya Rwanda na Yugoslavia (IRMCT) iliyoko chini ya umoja wa taifa. Anasema kwamba, ndani ya Afrika Kusini pekee, imezichukua takribani mwaka mmoja, mamlaka na kikosi maalum cha umoja wa mataifa kufuatilia mienendo ya Fulgence Kayishema ambapo walitumia takribani miezi kumi kukusanya taarifa kutoka kwa watu ambao walikuwa wanaangaliwa kwamba wanamsaidia mtuhumiwa kujificha na kutoroka mkono wa sheria. Aidha walitumia utaalam wa kisasa wa upelelezi ikiwemo uchambuzi wa mawasiliano ya simu, uchunguzi wa miamala ya kifedha na mbinu nyingine.
Nilipomuuliza kuhusu ni kwa nini imechukua muda mrefu wa zaidi ya miaka ishirini hadi kufikia kumtia mbaroni Fulgence Kayishema, bwana Serge Brammertz anafafanua akisema, "Mojayapo ya shida ni dhahiri kwa watuhumiwa wengi, waliojificha katika nchi za kiAfrika, ni kwamba walitumia vibaya utambulisho bandia na kujificha na hata mara nyingi zaidi kati jamii ya wakimbizi.
Tukimtazama Kayishema kama unavyojua, alihusika kwa kiasi kikubwa katika kufanya mauaji ya kimbari. Kisha akakimbilia DRC. Kutoka hapo akaenda Tanzania, alienda kwenye kambi za wakimbizi huko. Alihamia Msumbiji kwenye kambi nyingine ya wakimbizi. Kisha alikaa muda huko Eswatini kabla mwishoni wa miaka ya tisini kuhamia Afrika Kusini. Wakati huo huo alikua ametumia hati nne tofauti za kusafiria, vitambulisho tofauti, alikuwa hata anapata hati ya ukimbizi wakati huo katika nchi tofauti. Kwa hivyo, hoja ninayotaka kusema ni rahisi sana kupata hati bandia. Ni vigumu sana kwa mamlaka ya kufanya uthibiti wa namna hii. Hasa ikiwa una idadi muhimu ya watuhumiwa walio mafichoni. Na hivyo ndivyo alivyoweza kujificha kwa miaka mingi katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini."
Na kuhusu atakakopelekwa mtuhumiwa huyu wa mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda, Mwendesha Mashitaka Serge Brammertz ananiambia kwamba Afrika Kusini wameanza mchakato wa kisheria. Kisha ombi lililopo ni mtuhumiwa kupelekwa Arusha, Tanzania,
lakini wezekano mkubwa ni kwamba mashitaka na usikilizaji wa kesi itafanyika nchini Rwanda. "Kama unavyojua, tuko katika awamu hii ya mwisho ya ofisi ya Mwendesha Mashitaka ya Mfumo wa Kimataifa wa kushugulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari. Pia, Baraza la Usalama limetuhimiza kuhakikisha kwamba kesi zote zilizosalia zinasikilizwa na ofisi za mashitaka na yeye anayepaswa kufanyiwa hivyo katika taasisi za Rwanda."
Mnamo mwaka wa elfu mbili na moja (2001) Fulgence Kayishema, alishitakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa nchini Rwanda, ICTR, iliyokuwa Arusha, Tanzania kwa makosa ya mauaji ya kimbari, kufanyikisha mauaji ya kimbari, kuchochea mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu kwa mauaji na makosa mengine yaliyofanyika katika kitongoji cha Kivumu, jimbo la Kibuye. Inadaiwa kuwa tarehe kumi na tano (15) mwezi wa Aprili mwaka elfu moja mia tisa tisini na nne (1994), Kayishema pamoja na watuhumiwa wengine, waliwaua zaidi ya watu elfu mbili kwenye kanisa huko Nyange. Na inadaiwa kuwa alishiriki mmoja kwa mmoja katika kupanga na utekelezaji wa mauaji hayo, ikiwa ni kununua na kusambaza petroli na kuchoma moto kanisa ilihali watu wakiwa ndani na hata waliobaki hai bada ya moto walikufa baada ya wauaji hayo kutumia tingatinga kuangusha kanisa lote.
Watuhumiwa wengine watatu bado wanasakwa ili wakutane na mkono wa sheria.